Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kutumia mifumo ya kidijitali katika uendeshaji na uchakataji wa taarifa za wanachama ili kuboresha utendaji na utunzaji wa taarifa za kifedha.
Mrajis ametoa kauli hiyo leo Juni 21, 2024 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa TEHAMA wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo SCCULT (1992) Ltd kwa ajili ya uendeshaji na utoaji huduma za vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).
Akiongea katika uzinduzi huo, ameelekeza Muungano wa Vyama vya Ushirika wa kifedha (SCCULT) kuhakikisha mfumo huo una uwezo wa kusomana na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaosimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tume inapata taarifa za vyama kwa ajili ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya ushirika.
Akisisitiza kuwa utekelezaji wa uendeshaji wa vyama vya ushirika kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ni sehemu ya maono makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inahitaji vyama vya ushirika kuwanufaisha wanachama na kukuza uchumi, Dkt. Ndiege alisema TEHAMA inatumika kama chachu ya kuongeza tija, uwazi na kasi ya uchumi.
Makamu Mwenyekiti wa SCCULT, Kolimba Tawa, amesema mfumo huo unaenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa taarifa za vyama, utaongeza uwazi na uwajibikaji kutokana na taarifa kuchakatwa na zaidi ya mhusika mmoja, kutengeneza ripoti zinazohitajika na wadau kwa wakati pamoja na upatikanaji wa kumbukumbu hasa panapojitokeza changamoto.
Mfumo huo wa TEHAMA wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo SCCULT (1992) Ltd umeundwa kwa kushirikisha Kampuni ya UBX, Umoja Switch, DSIK pamoja na vyama mbalimbali vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).
Umuhimu wa Mfumo wa TEHAMA kwa SACCOS
Mfumo huu wa TEHAMA una umuhimu mkubwa katika SACCOS kujiendesha kidijitali kwa sababu mbalimbali:
- Ufanisi na Usahihi: Mfumo wa kidijitali unarahisisha na kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku za SACCOS, kupunguza makosa ya kibinadamu na kuhakikisha taarifa zote muhimu zinapatikana kwa urahisi na haraka.
- Upatikanaji wa Taarifa kwa Wakati: Wanachama wa SACCOS wataweza kupata taarifa zao binafsi na za kikundi kwa wakati kupitia mifumo ya kidijitali, hivyo kuongeza uwazi na uaminifu katika uendeshaji wa shughuli za SACCOS.
- Kupunguza Gharama za Uendeshaji: Mfumo wa TEHAMA unasaidia kupunguza gharama za uchapishaji wa nyaraka na usafirishaji wa taarifa, kwani kila kitu kinaweza kufanyika kidijitali.
- Usalama wa Taarifa: Mfumo wa kidijitali unajumuisha viwango vya juu vya usalama wa taarifa, hivyo kuhakikisha kuwa taarifa za wanachama na shughuli za SACCOS zinalindwa dhidi ya udanganyifu na upotevu.
- Kuboresha Huduma kwa Wanachama: Kwa kutumia teknolojia, SACCOS zinaweza kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake, ikiwa ni pamoja na mikopo ya haraka, ufuatiliaji wa malipo, na ushauri wa kifedha kwa njia ya mtandao.
- Kuendana na Mabadiliko ya Teknolojia: Mfumo huu unazifanya SACCOS ziweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea ulimwenguni, hivyo kuziwezesha kushindana kwa ufanisi katika sekta ya fedha.
- Utunzaji Bora wa Taarifa: SCCULT kama mwamvuli wa vyama vya akiba na mikopo inahakikisha usalama wa taarifa za wanachama katika mfumo kwa kurahisisha upatikanaji na utunzaji wa taarifa muhimu za wanachama. Mfumo huu unaruhusu kuhifadhi taarifa kwa njia salama na rahisi kufikiwa wakati wowote inapohitajika, hivyo kuimarisha uaminifu na utulivu wa shughuli za SACCOS.
SCCULT: JUMUISHI KWA USTAWI WA SACCOS